Licha ya halmashauri ya kutoza ushuru nchini kra kutangaza kukusanya mabilioni ya fedha kama ushuru, waKenya wengi wamelalamika kuhusu ufisadi kumea mizizi na kukolea katika halmashauri hiyo. Na ukidhani kwamba mambo yapo katika halmashauri ya ushuru tu, basi umekosea, kwani labda ngoma yenyewe haswa ipo katika bandari ya Mombasa. Licha ya kuwepo kwa wafanyibiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje na kulipia ushuru kama inavyohitajika, uchunguzi wa jicho pevu la ktn uliochukua jumla ya miezi minne umebaini kwamba mambo ya mizengwe bandarini nayo yapo kwa wingi. Ili kubaini ukweli wa mambo mwanahabari wako mpekuzi Mohammed Ali akishirikiana na mwenzake John Allan Namu waliamua kufungua kampuni na kuagiza bidhaa kutoka ngambo kubaini ikiwa kweli ni rahisi kukwepa kulipia ushuru. Waswahili watakwambia utamu wa ngoma ni uingie ndani ucheze, hapa ktn tunasema kwa uhondo kamili kuhusu jinsi ngoma ilivyochezwa tulia tuli mambo yalipangika na kupanguliwa katika bandari ya Mombasa pamoja na halmashauri ya kutoza ushuru nchini kra. Makala ni Zengwezengwe Bandarini Sehemu Ya Kwanza.