Ni miaka miwili sasa tangu Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga waliposalimiana nje ya jumba la harambee na kutia saini makubaliano ya kuunda serikali ya muungano. Tukio lenye umuhimu mkubwa mno ambao hauwezi kusahaulika kwani ulikomesha ghasia zilizokuwa zikiendelea mfano wa dereva anayeshika breki za dharura akiwa katika mwendo wa kasi. Lakini visa vya hivi majuzi vya kupatikana kwa silaha mikononi mwa watu binafsi mjini narok mkoa wa Rift Valley vimeibua hofu kuu. Baadhi ya maswala yanayowatatiza wakenya wapenda amani ni je, kuna uwezekano kwamba kuna baadhi ya makundi yanayolenga kuzua ghasia kwa mara nyingine. Ili kubaini ukweli wa mambo mwanahabari mpekuzi muhammed ali alizama katika mkoa wa Rift Valley kutafuta hali halisi ya mambo. Na kama utakavyoona katika taarifa hii, serikali inapaswa kuwa macho kwani kuna uwezekano wa historia kujirudia na kuwaacha wakenya na maafa makubwa. Kwa taarifa kamili hii hapa sehemu ya kwanza ya makala ya demokrasia kijambazi. Tungependa kukuonya mtazamaji kwamba baadhi ya picha katika taarifa hii ni za kutatiza.